Na idrisa bandali
Azam fc wamepania kuifunga Simba SC leo
katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam ili kupanda kileleni mwa ligi hiyo.
Kocha Boris Bunjak kutoka Serbia
amekuwa akiwaandaa vizuri vijana wake kwa mazoezi na kisaikolojia pia kuelekea
mchezo huo, unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.
Azam ipo kambini kwake, Chamazi
ikijifua vikali na wachezaji wameweka kambi hapo, kwa ajili ya Ligi Kuu.
Kiboko ya nyavu za Simba na Yanga,
John Raphael Bocco ‘Adebayor’ yuko fiti kupita maelezo na kiungo bora Afrika
Mashariki na Kati kwa sasa, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliyekuwa majeruhi
mwanzoni mwa msimu sasa amepona kabisa.
Kiungo Abdulhalim Humud aliyekuwa
anasumbuliwa na maumivu katika mechi tatu zilizopita kwa sasa yuko fiti kabisa
na habari njema zaidi ni kwamba, kiungo mwingine Mzanzibari Abdi Kassim
‘Babbi’ amerudi kwenye fomu na anafumua mashuti makali na ya mbali ya hatari.
Viungo washambuliaji kutoka Ivory
Coast, Kipre Herman Tcheche na Kipre Michael Balou wote wapo fiti sawa na
makipa Deo Munishi ‘Dida’, Mwadini Ally, mabeki Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni,
Said Mourad na Aggrey Morris.
Kwa ujumla Azam iko tayari kwa mechi
hiyo ya leo ambayo wamepania kushinda ili kulipa kisasi cha kufungwa na Simba
katika Kombe la BancABC Sup8R.
Simba yenyewe inaendelea vizuri na
kambi yake visiwiani Zanzibar kujiandaa na mchezo huo na inatarajiwa kurejea leo
mchana na moja kwa moja kuelekea
uwanjani kukipiga.