Kikosi cha Simba |
Na idrisa bandali
Wekundu wa Msimbazi, Simba SC
wanatarajiwa kurejea Leo Dar es Salaam wakitokea Zanzibar ambako waliweka kambi
ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa wa leo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
dhidi ya Azam FC, Uwanja wa Taifa.
Pamoja na Juma Nyosso na Haruna
Moshi kusimamishwa, lakini wachezaji waliobaki wana morali ya hali ya juu na
wamepania kushinda mechi ya kwanza kati ya nne, baada ya sare nne mfululizo.
Kwa kawaida Simba SC huenda Zanzibar
katikati ya Ligi Kuu kuweka kambi linapokaribia pambano dhidi ya mahasimu wao
wa jadi, Yanga SC lakini kwa kitendo cha kwenda kujichimbia huko kwa ajili ya
Azam, maana yake wanaipa uzito huo mechi hiyo.
Simba ilienda Zanzibar Jumanne, siku
moja baada ya kurejea kutoka Tanga, ambako ililazimishwa sare ya bila kufungana
na wenyeji Mgambo JKT Jumapili katika mfululizo wa ligi hiyo.
Matokeo hayo, yaliifanya Simba
ifikishe pointi 19, baada ya kucheza mechi tisa na kuendelea kuongoza Ligi Kuu.
Awali ya hapo, Simba ilitoka 2-2 na
Kagera Sugar Uwanja wa Taifa na 0-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani.
Baada ya sare ya Jumapili,
Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage amewataka wanachama na wapenzi
wa klabu hiyo kuwa watulivu na wasikatishwe na tamaa na sare tatu mfululizo za
timu hiyo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwani safari bado ni ndefu.
Rage amesema kwamba, hadi sasa timu
yao haijafungwa katika Ligi Kuu kuashiria kwamba bado ni timu bora na matokeo
ya sare hizo tatu mfululizo pia ni kutokana na uimara wa timu yao.