Na idrisa bandali
BEKI Kevin Yondan na mshambuliaji
Said Bahanuzi waliokuwa nje ya Uwanja kwa zaidi ya wiki mbili kutokana na
kusumbuliwa na majeruhi, leo wanatarajiwa kuanza programu rasmi ya mazoezi na
wenzao baada ya kupata ahueni ya kutosha.
Wachezaji hao wamekuwa wakifanya
mazoezi mepesi kwa zaidi ya wiki moja baada ya kupata ahueni kidogo na sasa
wamepona kabisa na leo kocha Mholanzi, Ernie Brandts anatarajiwa kuwajumuisha
kwenye programu yake kamili, Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es
Salaam.
Yanga imerejea kutoka Arusha, ambako
Jumamosi ilivuna pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji JKT
Oljoro, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kupanda nafasi ya pili kwenye msimamo wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, wakitimiza pointi 20 baada ya kucheza mechi
10.
Yanga sasa iko nyuma kabisa ya
wapinzani wao wa jadi, Simba SC wanaoongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 22, baada
ya kucheza mechi 10 pia.
Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na
Kati, Kombe la Kagame sasa wanajiandaa na mchezo wao ujao wa ligi hiyo, dhidi
ya Mgambo JKT Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mgambo JKT pamoja na kwamba imepanda
Ligi Kuu msimu huu, lakini imeonyesha ni timu ya ushindani baada ya kutoa sare
ya bila kufungana na Simba SC, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kwa sababu hiyo, Yanga wamechukua
tahadhari ya kutosha kuelekea mchezo huo na tangu jana Mwenyekiti wa Kamati ya
Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb amekuwa ‘akienda mbio’ kuhakikisha
timu inashinda keshokutwa.
Kurejea kwa Yondan na Bahanuzi
kunaongeza matumaini ya ushindi kwa Yanga katika mchezo huo, ingawa upande
mwingine ni mtihani kwa Brandts, kwani katika kipindi ambacho wachezaji hao
wako ‘wadini’, walioshika nafasi zao wamekuwa wakifanya vizuri.
Mbuyu Twitwe aliyehamishwa kutoka
beki ya kulia hadi beki ya kati tangu Yondan aumie Oktoba 3, amekuwa akifanya
vizuri sawa na Jerry Tegete aliyempokea Bahanuzi Oktoba 8, alipoumia naye
amekuwa akifanya vizuri pia.
Kwa kuzingatia Twite alikuwa
‘uchochoro’ alipokuwa akicheza pembeni, watu wanasubiri kuona kama Brandts
atamrudisha huko huko baada ya Yondan kurejea, au ataamua mmoja kati yao na
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ataanzia benchi.
Upande wa Tegete na Bahanuzi, kuna
uwezekano mmoja wao atakuwa anaanzia benchi kwa sasa na mwingine kumpokea
mwenzake baadaye.