Monday, August 5, 2013

Mwinyi awaomba radhi watanzania kwa kutorokea umangani

Wiki kadhaa baada ya kutoroka nchini na kukimbilia nchini Qatar kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio ya soka la kulipwa, leo hii kiungo wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya Simba Mwinyi Kazimoto amezungumza rasmi na mtandao huu na kutoa taarifa nzima ya kuhusu sakata lake la kutoroka.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Doha Qatar na Shaffih Dauda, Mwinyi Kazimoto kwanza amekiri kwamba alitoroka kwenda Qatar kwa nia ya kwenda kufanya majaribio, "Safari yangu ya kuja huku Qatar ilibidi iwe kabla hata sijacheza mechi ya marudiano na Ivory Coast, lakini kwa sababu nilikuwa na majukumu nilivumilia nikabaki mpaka nilipocheza mchezo wa kwanza dhidi ya Uganda, wakati tukiwa kambini kwa ajili ya mchezo wa pili ikabidi niondoke kwa sababu siku zilikuwa zinaenda na muda wangu wa kufanya majaribio ukawa unaisha," anazungumza Kazimoto

Alipoulizwa kama tayari ameshafuzu majaribio aliyoenda kufanya kiungo huyo wa zamani wa JKT Ruvu alisema: "Mwanzoni nilipata vilabu viwili vinavyoshiriki ligi daraja la kwanza ya huku, lakini nikachelewa majaribio na hivyo nikakosa nafasi. Baada ya hapo ndipo ikajitokeza timu ya Al-Markhiya Sports Club - inayoshiriki ligi ya daraja la pili na ikavutiwa nami na ikafanya mipango ya kunisajili."

Taarifa nchini zimeenea kwamba klabu ya Simba imepokea kiasi cha $35,000 kwa ajili ya kumuuza kiungo huyo, Je Kazimoto anasemaje juu ya hili? "Ni kweli kutokana na kwamba nilikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na Simba ilibidi nitoe kiasi cha fedha ($40,000 na sio $35,000 kama inavyoripotiwa) kutoka kwenye ada ya usajili wangu kuununua mkataba wangu uliobakia na Simba.


"Sasa hivi nimefanikiwa tayari kupata timu hii lakini ndoto yangu ni kujitahidi na kuweza kucheza ligi ya juu kabisa hapa. Vilevile ningependa kuwaomba radhi watanzania wote na klabu yangu ya Simba kwa kitendo cha kutoroka wakati nikiwa nahitajika. Nafasi ya kucheza soka la kulipwa ilikuwa ni muhimu kwa maisha yangu na sikutaka niipoteze hivyo naomba wanielewe na kunisamehe."(habari hii ni mali ya shaffih dauda.blogsport.com)