Siku
ya vijana duniani, serikali imeainisha mikakati na sera za kuwakwamua vijana?
Nilikuwa kimya nikisikiliza na kufuatilia kwa makini
matamko au hutuba zenye mantiki kwa vijana wa Tanzania kutoka serikalini.
Nilianza kwa kuingia mtandaoni labda kunachochote nikakaa karibu na redio na
kila wakati wa habari nilibadilisha kituo mara hiki mara kile ilimladi nisikie
hotuba ya kiongozi yeyote wa serikali akitamka jambo kwa vijana ambao ni nguvu
kazi ya taifa lolote duniani. Mpakailipo malizika taarifa ya habari ya
saa mbili usiku ya moja ya redio kubwa hapa nchini ndipo nilipo pandisha na kushusha
pumzi na kuanza kufikiri kwa kina zaidi.
Hivi serikali, taasisi na idara zake haitambui siku
ya vijana duniani? Na kama inatambua inaienzi vipi siku hii? Au inaitumiaje? Au
ndio haifanyi maadhimisho mpaka waisani mashirika yasio ya kiserikali yanayojihusisha
na mambo hayo yaoneshe nia na kuadhimisha siku hiyo kwa ushirikiano na serikali
kama tunavyoambiwaga? Hapa naizungumzia serikali ngazi ya Wizara na Idara makao
makuu, lakini kule mikoani katika ofisi za Katibu tawala wa mikoa kuna wataalam
walioajiriwa miaka ya hivi karibuni kama watu wanaoshughurikia maswala ya
michezo na maendeleo ya vijana. Hawa tutasema wapo chini ya serikali kuu hawana
bajeti ya maendeleo, na vipi katika ofisi za Wakurugenzi wa halmashauri zetu?
Kama wanamipango wanatumia wakati gani kutoa taarifa kwa
watu wa kawaida? Kama ipo na ni hafifu, wataalam watasema vipau mbele, ama
mipango tuliopanga kwa mwaka wa fedha haikupitishwa, niwakati gani sisi vijana
tutajua haya? Amana katika mbao za matangazo pale halimashauri ni matangazo ya
kawaida tu, tunashukuru kwayo maana tukitaka taarifa hizo tunazipata hapo. Ama
taarifa hizi za utekelezaji wa maendeleo kwa vijana na mipango yake au
sera zinazomuwezesha kijana hasa kijana wa kawaida tunazipata wapi?
Hivi sasa Tanzania kunajuhudi kubwa za
utumiaji(Utilization) ya mali asili kama Gesi, Madini, Bahari, Maziwa na Mito.
Katika Gesi peke yake nina imani kuwa vijana wengi waliosoma na wasio soma
wanaweza kupata fursa, Madini halikadhalika na Maji kwa maana ya mito, maziwa
na Bahari kwa mfano halimashauri zilizo chini ya mamlaka ya kuliendeleza bonde
la mto kilombelo zimejipanga vipi kujenga fursa kwa vijana waishio katika mradi
ulio chini ya mamlaka hizi? Wanatumia muda gani kuwafahamisha vijana fursa
zilizopo au zinazokuja kupitia mipango hii mikubwa ya maendeleo ya serikali?
Mimi nilifikili fursa hizi zilizopo na zinazokuja serikali ingeweka kipaumbele
hasa nafasi za ajira na fursa zinazotokana na mipango kama hii kwa vijana, na
siku za maadhimisho ya siku ya vijana duniani, Halmashauri kama Halmashauri au
Mkoa kama Mkoa hata serikali kuu kwa ujumla inatumia nafasi ya siku kama hii
kuelezea Mipango ya maendeleo kwa vijana iliyokwisha kutekelezwa au iliyopangwa
kutekelezwa, hata kama kuna fursa vijana inabidi wapewe taarifa hii kwa lugha rahisi
kwa kuwa ni haki yao ya kikatiba kupata taarifa.
Mamlaka zote zimekaa kimya najua kutakuwa na majibu mengi
ya kisiasa, hatukuwa na bajeti, vipau mbele vilivyopitishwa ni vya shughuli za
maendeleo tu na sio maadhimisho ya siku yoyote ile. Lakini hawa watu
maalum(Focal Person) ambao ni wataalam mliowaajiri kazi yao ni nini? Je vijana
wanataarifa ya sababu hizo? Je wameshirikishwa na imeshindikana? Na ninyi
watumishi wa serikali mnaonaopewa dhamana hii mnafikiri vipi? Kuna fursa
nyingi sana hata haziitaji kasma ya serikali kufanya shughuli ndogo kama hizi.
Ndipo nikaona kuwa UWAZI na
UWAJIBIKAJI unatafsiri pana sana na kwa muktadha huu maswala makubwa haya
katika serikali zetu hayapo na kama yapo sio kwa kundi kubwa kama la ndugu
zangu waliopo Kule Mtimbira, Ngoilanga au Kilosa kwa Mpepo Wilaya ya Mahenge
Ulanga au kule kwa watani wangu Mpapura, Naumbu au Msanga Mkuu Wilaya ya Mtwara
Vijijini. Vijana wa maeneo haya wanapata taarifa hizo kwa urahisi kiasi gani na
wakafaidika kwa kiasi cha kuonekana?. Imani yangu ni kuwa uwepo wa vyombo vya
habari kila kona ya nchi hii ingesaidia kama sio barua maalum kutoka mamlaka za
serikali basi maafisa wahusika wangekuwa angalau na kipindi redioni hasa katika
vituo vya redio zilizopo huko na vijana wakapata wasaa wa kuuliza maswali na
kujibiwa, mpango huu haugharimu chochote si kwa serikali au kwa afisa wa
serikali. Ndio maana nasema kwa muktadha huu maswala ya UWAZI na UWAJIBIKAJI
katika Serikali na Halmashauri zetu haupo. Na kwa maana hii vijana wanatumiwa
tu pale wanapohitajika lakini wao wanapo hitaji hawana wa kumkimbilia.
Kilio changu ni kwa vijana masikini na wasiosoma waliopo vijijini na mijini
hawa serikali inawaambia nini? Hasa siku hii ya vijana duniani, Tanzania
inaadhimisha kwa namna gani? Maana hili ndilo kundi kubwa na ndilo kundi
litakaloleta taharuki(Political instability or social unrest) kama serikali
haitaweka mikakati maalum ya kulikomboa kundi hili, tumeanza kuona mikakati ya
ajira kama ajira zilivyotoka hivi karibuni au kupelekwa JKT kwa vijana
ambao wamefaulu, tunashukuru sana. Lakini utaona vijana ambao hawakupata
fursa ya kusoma hawapo katika mikakati hii miwili, siku hii ya Vijana serikali
ingesema kitu kwa kuwa kutoa ajira kwa waliosoma na kuwapeleka JKT waliofaulu
tu ni sehemu tu ya utatuzi wa kero za vijana hapa nchini na tukumbuke
kuwa wasomi wanahafadhali kidogo hata wangeachwa, kuliko kuwaacha hawa ambao
hawakusoma shida yake ni kubwa leo na hata siku zijazo. Tumeanza kuona kundi
hili la vijana likitumika kwa migomo na vurugu mbalimbali mikoani, na naona
jinsi usalama wan chi utakavyolegalega siku chache zijazo mpaka tutakapo maliza
mchakato wa katiba na uchaguzi mkuu, nahakika asilimia tisini ya vijana
watakaotumiwa na watu wenye nia mbaya na nchi hii ni kundi hili la vijana.
Kupunguza yote haya ambayotunaona yanatokea na yanaelekea kuendelea kutokea,
siku hii ya Vijana duniani ingeadhimishwa hapa Tanzania na Serikali angalau ingetutangazia au kuja na mpango wa dharula
wenye lengo la kuwakwamua vijana wa Tanzania ingechangia kwa kiasi kikubwa
kupunguza taharuki kizi.
Maoni yangu ni kuwa Wanaharakati, wanasiasa na serikali
kwa ujumla naamini kuwa sisi sote tuna mipango na mikakati ya kuwakwamua
na kuwaendeleza vijana, kila mmoja wetu angetokea kuazimisha siku hii na kusema
atawatendea nini vijana ili vijana walijenge taifa lao na maisha yao na familia
zao.
Tumesikia katika vyombo vya habari jana(12/08/2013)
Serikali ya uingereza imeshauriwa na kambi ya upinzani kuwa Makampuni yote ya
kigeni na yale ya ndani kwanza yaweke kipaumbele cha ajira kwa wazawa, waziri
kivuli wa Mambo ya Uhamiaji wa uingereza Mr Chrisbrant alidiliki hata kutaja
majina ya kampuni zinazotoa ajira kwa wingi kwa wageni. Sisi kwetu je?
Tunashindwa nini? Mbona ni swala la Kukopi na kupesti tu. BAVICHA ilibidi
watamke kitu juu ya siku hii kwa namna rahisi kabisa, UVCCM hali kadhalika na
Serikali pia, mashirika yasiyo ya serikali ya vijana kama TYC na mengine
mengi.
Kwetu vijana tunafursa gani au tumepangiwa na
kushirikishwa kupanga nini kwa maendeleo yetu? HAKUNA KITU wala HAKUNA TAARIFA
YEYOTE kama ipo basi haifikiki au kueleweka kirahisi kwa kundi kubwa hili la
vijana ambao hawakupata fursa ya kwenda shule na hivi sasa wamebaki
wakiyumbishwa na wajanja huku serikali inaona wananchi hawa
wakiteketea na madawa ya kulevya, kufungwa kutokana na ujambazi, ugaidi hata
uchochezi na ushiriki wa kuvuruga amani ya nchi. Nashauri vijana tuzitumie
fursa zinazojitokeza kikamilifu na tujitahidi kuto hadaika na wajanja
wanaotulubuni kwa manufaa yao wenyewe. Ili amani idumu serikali hainabudi
kuweka mikakati endelevu na makini sana kwa kundi hili la vijana, ni matumaini
yangu kuwa wadau wote watakuwa wamepata wazo hili na kuliingiza katika mikakati
na mipango yao ya maendeleo kwa mwaka unaokuja ili kuweka mambo sawa na wote
tukaweza kufaidi Neema za nchi kama zilivyoletwa na mwenyezi mungu na sio
wakafaidi wachache tu.