Serikali ya
Tanzania imesema inatafakari ushiriki wake ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
na inaweza kujitoa ndani ya Jumuiya hiyo iwapo itaendelea kutengwa katika
baadhi ya vikao.
Aidha
imesema Tanzania haitambui vikao vinavyofanywa na nchi tatu zilizopo ndani ya
Jumuiya hiyo ambazo zimekuwa zikizitenga Tanzania na Burundi.
Waziri
anayehusika na masuala ya Afrika Mashariki wa Tanzania Samwel Sitta ameliambia
Bunge la Tanzania kuwa makubaliano ya vikao hivyo vinavyofanywa na nchi za
Kenya, Rwanda na Uganda yatatekelezwa na nchi hizo zinazofanya vikao hivyo kwa
sababu vinafanyika nje ya utaratibu wa mkataba wa jumuiya hiyo
Katika
mikutano iliyofanyika hivi karibuni Tanzania na Burundi hazikualikwa kwenye
vikao hivyo.
Kwa mujibu
wa Waziri Sitta mikutano ya wakuu wa nchi za Rwanda, Kenya na Uganda ambayo
ilianza kwa kuitenga Tanzania ilifanyika Entebbe nchini Uganda mwezi Juni mwaka
huu na kufuatiwa na mkutano wa pili uliofanyika Agosti mwaka huu huko Mombasa
nchini Kenya ambapo nchi hizo tatu bila kuishirikisha Tanzania walizungumzia
uanzishaji wa himaya moja ya forodha.
Mambo
mengine waliyozungumza wakuu hao ilikuwa uanzishaji wa visa moja ya utalii kwa
nchi zao na matumizi ya vitambulisho vya uraia ambavyo vitatumika kama hati za
kusafiria miongoni mwa nchi hizo.
Aidha Waziri
Sitta amesema ndani ya mikutano hiyo pia walizungumzia kuanzisha mchakato wa
kuanzisha shirikisho la nchi hizo.
Tayari
Tanzania imeanza mazungumzo na nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo kuangalia ni kwa namna gani zitaanzisha ushirikiano nje ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki kama zinavyofanya nchi za Rwanda, Uganda na Kenya