Wizara ya Maji ikishirikiana na OWM -TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya mbalimbali zimepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa kwa kuwapatia maji wananchi waishio vijijini wapatao 752,000 wa ziada katika kipindi cha miezi mitatu tangu tarehe 1 Julai mwaka huu.
Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 2 ya wakazi wote wanaoishi vijijini kupata huduma ya maji safi kwa kipindi hicho cha miezi mitatu. Baadhi ya miradi iliyokamilika ni ya vijiji vya Mtandi, Rondo, na Kineng’ene vilivyopo Mkoani Lindi; Vijiji vya Engagile, Gedamar, Mtuka vilivyopo Mkoani Manyara; na Vijiji vya Iwalanje, na Maninga vilivyopo Mkoani Mbeya. Hivi ni baadhi tu ya vijiji ambavyo miradi imekamilika na wanavijiji wanapata huduma ya majisafi na salama karibu na makazi yao.
Akizungumzia mafanikio hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Christopher Sayi amesema “Nina imani kubwa tutadumisha usambazaji wa maji safi na salama kwa wananchi 15,200,000 ndani ya kipindi kilichopangwa cha miaka mitatu ya utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (MMS) kuanzia 2013/2014 hadi 2015/2016”
Mafanikio haya yamewezekana kutokana na MMS kugatua madaraka kwa watendaji, jambo ambalo limewafanya watendaji kuwajibika na kuharakisha utendaji wao wa kazi za kila siku. Katika kuhakikisha mafanikio ya MMS na kutimiza lengo, Wizara ya Maji imeongeza ufanisi katika masuala ya ununuzi wa huduma, ikiwemo ujenzi na vifaa vyake, kutoka siku 265 za hapo awali hadi siku 90 za sasa.
Aidha Afisa Mwandamizi katika Wizara hiyo, Mhandisi Goyagoya Mbenna, alisema “Mpango huu wa MMS umetuwezesha sisi Wahandisi kufanya kazi kwa umakini na umeleta mafanikio katika kuharakisha utendaji wetu wa kazi”
Kwa upande wake Bwana Omari Issa, Mtendaji Mkuu wa PDB alisema, “Nimefurahi sana kuona utaratibu huu wa MMS umepokelewa vizuri na watendaji na wananchi. Nawashauri wahusika wote waendelee kuufuatilia na kuutekeleza kwa makini kwa kuwa unaleta fursa ya kipekee ya kuleta maendeleo ya haraka nchini mwetu”.
Hapo awali ongezeko la idadi ya wananchi wanaopata huduma ya majisafi vijijini ilikuwa ni kati ya asilimia 0.5 hadi 1.0 kwa mwaka, sawa na ongezeko la watu kati ya 300,000 – 500,000 kwa kipindi hicho. Kwa kupitia mfumo huu wa sasa wa MMS, Wizara ya Maji itatekeleza jumla ya miradi 1,810 (sawa na vituo 26,720 vya kuchotea maji) na kuunda vyombo vya watumia maji 2,728 nchi nzima kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2013/2014 – 2015/2016. Miradi hii itazidisha usambazaji wa maji kwa wakazi 7,000,000 waishio vijijini ili jumla ya wananchi 22,300,000 ambayo ni sawa na zaidi ya asilimia 67 ya wakazi wote vijijini wawe wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao ifikapo Juni 2016.
Hadi kufikia mwezi Septemba 2013, jumla ya vituo vya kuchotea maji 3,008 vimekamilika na kutoa huduma ambapo jumla ya wakazi 15,952,000 vijijini wanapata huduma hiyo ya maji safi. Aidha, vyombo vya watumia maji 228 vimeundwa na kuanza kufanya kazi. Wizara ya Maji ikishirikiana na OWM- TAMISEMI, Halmashauri inaendelea na ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya maji pamoja na shughuli za uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji katika vijiji mbalimbali nchini. Kwa kulingana na juhudi zinazoendelea Matokeo Makubwa yatapatikana kama ilivyokusudiwa.
Mara kwa mara Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe amekuwa akiwataka wafanyakazi wa sekta ya maji kuhakikisha wanaongeza jitihada katika kazi sambamba na kwenda na kasi ya MMS. Katika kikao chake cha hivi karibuni na wafanyakazi wa Wizara ya Maji alisema, “Sitaki yale maneno ya kawia ufike, mwendapole hajikwai” Sisi tunasema “Haraka haraka ndiyo mwendo”. Hivyo nataka tufanyekazi kwa bidii, na kwa ufanisi wa hali ya juu” Alisisitiza Waziri.
Wizara ya Maji kwa upande wake inashirikiana na OWM-TAMISEMI kusimamia na kufuatilia utekelezaji ili kujiridhisha kuwa miradi ya Maji inatalekelezwa kwa kiwango kilichowekwa.