Mbunge wa
Nzega, Dk Khamis Kigwangalla, (CCM), leo anatarajiwa kuanza kukusanya saini za
wabunge akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya kutokuwa na imani na Spika wa
Bunge, Anne Makinda kwa madai kwamba amekuwa akikiuka kanuni za Bunge.
Dk
Kigwangalla aliibua hoja ya kutokuwa na imani na Spika katika kikao cha wabunge
wote cha kuelezea shughuli zitakazofanywa na Bunge katika mkutano wa 13,
kilichofanyika juzi jioni kwenye ukumbi wa Pius Msekwa.
Mbunge huyo
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, jana alithibitisha kuwapo kwa mjadala huo katika kikao cha wabunge,
lakini hakuwa tayari kueleza kwa undani na badala yake alisema kwamba leo
ataanza kukusanya saini za wabunge kwa ajili ya kukamilisha hoja ya kutokuwa na
imani na Spika Makinda.
Chanzo chetu
kutoka katika kikao hicho cha wabunge kilibainisha kuwa Kigwangalla alihoji
kuhusiana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge
(CCM-Bariadi Magharibi) kuteuliwa na Spika wakati katika kamati nyingine
wenyeviti na makamu huchaguliwa na wajumbe wa kamati husika.(P.T)
Pia Dk
Kigwangala alisema Spika Makinda alivunja kanuni kwa kuwapa posho ya Sh430,000
kwa siku wajumbe wa kamati inayoongozwa na Chenge wakati wajumbe wa kamati
nyingine wamekuwa wakipewa Sh130,000.
"Anachokifanya
Spika ni matumizi mabaya ya fedha za umma, inakuwaje wengine wafanye kazi hata
bila posho lakini wao (Kamati ya Bajeti), walipwe posho ya Sh430,000 kwa
siku?" chanzo hicho kilimkariri Dk Kigwangalla akihoji.
Hata hivyo,
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah akizungumza na gazeti hili jana alisema
mazingira ya kamati fulani kupata malipo ya ziada tofauti na viwango vya
kawaida hutokea pale uongozi wa kamati husika unapoomba kwa Spika.
"Si
kweli kwamba Kamati ya Bajeti inalipwa fedha za ziada kila wakati, hapana, ni
pale tu wanapoomba malipo hayo kutokana na sababu ambazo lazima Spika aridhike
nazo.
Ieleweke
kuwa siyo kamati hiyo tu, kwa sasa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ambayo
inachambua miswada mingi nayo imekuwa ikiomba na baada ya Spika kuridhia basi
nao wanapewa," alisema Dk Kashililah.
Katibu huyo
wa Bunge alieleza kuwa zaidi ya kamati nane zimewahi kuomba malipo ya ziada kwa
maana ya kutaka posho zaidi, ulinzi, usafiri na hata chakula, ikiwa
zinakabiliwa na majukumu ya ziada pia katika mazingira tofauti nje ya utaratibu
wa kawaida.
"Kimsingi,
kamati nyingi zinapewa malipo tofauti, watu wanaweza kuwa na kazi mpaka saa
saba au nane usiku, au wanakwenda kufanya kazi katika mazingira yasiyokuwa ya
kawaida, taratibu zinamruhusu Spika kama akiridhika na maelezo ya kazi husika,
basi anaruhusu kutekelezwa kwa maombi hayo," alisema Dk Kashililah.
Kuhusu
Serukamba
Aidha, Dk
Kigwangalla alinukuliwa akisema Spika amekiuka kanuni kwa kumchagua Mwenyekiti
wa Kamati ya Miundombinu, Peter Serukamba (Kigoma Mjini-CCM), kuwa mjumbe wa
Kamati ya Bunge ya Bajeti.
"Hakuna
mbunge yeyote aliyepo katika kamati mbili lakini hata kungekuwa na sababu
maalumu basi wa kuteuliwa angekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi,
Viwanda na Biashara, Mahmoud Mgimwa (Mufindi Kaskazini-CCM) ambaye TRA (Mamlaka
ya Mapato Nchini) ipo chini ya kamati yake," kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho
kilisema Dk Kigwangalla alisema badala ya kumweka karibu katika ushiriki,
Mgimwa alipokwenda katika kamati hiyo aliambulia kufukuzwa.
Akizungumzia
suala hilo, Dk Kashililah alisema Serukamba pamoja na wabunge wengine kadhaa
waliteuliwa na Spika kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kamati hiyo wakati wa
kipindi cha Bajeti Kuu ya Serikali.
Aliwataja
wabunge wengine walioteuliwa kushiriki katika Kamati ya Bunge ya Bajeti kuwa ni
John Cheyo (Bariadi Mashariki-UDP), Salahe Pamba (Pangani - CCM) na Hamadi
Rashid Mohamed (Wawi - CUF).
Kanuni za
Bunge
Kwa mujibu
wa kanuni za Bunge katika toleo la mwaka 2007, kifungu cha 137(1), ili
kumwondoa Spika madarakani, mbunge anayetaka kuwasilisha hoja hiyo atatakiwa
kuwasilisha taarifa ya maandishi ya kusudio hilo kwa Katibu, akieleza sababu
kamili ya kutaka kuleta hoja hiyo.
Kifungu
kidogo cha pili kinasema baada ya kupokea taarifa ya maandishi ya kusudio la
kumwondoa Spika kwenye madaraka, Katibu atapeleka taarifa hiyo kwenye Kamati ya
Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kujadiliwa.
Kifungu cha
tatu kinabainisha kuwa endapo kamati hiyo itaridhika kuwa zipo tuhuma mahususi
dhidi ya Spika zinazohusu uvunjaji wa masharti ya ibara husika za Katiba,
sheria au kanuni zinazoongoza shughuli za Bunge, basi kamati hiyo itaidhinisha
hoja hiyo ipelekwe bungeni ili iamuliwe.
Kanuni
zinasema Naibu Spika, atakalia Kiti cha Spika wakati wa kujadili hoja ya kutaka
kumwondoa Spika madarakani na Spika atakuwa na haki ya kujitetea wakati wa
mjadala na kwamba ili kumwondoa zinahitajika kura zisizopungua theluthi mbili
ya idadi ya wabunge wote.