|
Chuji |
KIUNGO wa
Yanga, Athumani Iddi ‘Chuji’ amesema kwamba Denizlispor FC waliyocheza nayo
jana mchezo wa kirafiki kilikuwa kipimo kizuri kwao, kwani timu hiyo ni nzuri
zaidi ya ile waliyocheza nayo awali, DSC Arminia Bielefeld ya Ujerumani.
Akizungumza naSWIRATY BLOG kutoka Uturuki jana, Chuji alisema kwamba mechi ya jana
imewasaidia sana kujua mapungufu na ubora wao kwa kuwa walicheza na timu nzuri iliyowazidi
uwezo.
“Hii timu ni
nzuri sana, kwa kweli imetupa changamoto nzuri na sisi wenyewe kama wachezaji
tumeona hicho kitu,”alisema Chuji.
Yanga SC jana
ilifungwa mabao 2-1 na Denizlispor FC ya Denizli, nchini Uturuki katika mchezo
wake wa pili wa kujipima nguvu katika ziara yake ya Uturuki, bao la kufutia
machozi likifungwa na Jerry Tegete.
Pamoja na
kufungwa na timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, iitwayo Bank Asya 1.
Lig, ambayo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya 10, imeelezwa Yanga
ilicheza soka ya kuvutia.
Denizlispor
Football iliyoanzishwa mwaka 1966, inatumia Uwanja wenye kuingiza mashabiki
19,500 wa Denzili Ataturk na mafanikio yake makubwa hivi karibuni ilikuwa mwaka
2002 waliposhika nafasi ya tano katika Ligi Kuu ya nchini humo na kufuzu kwenye
mchujo wa Kombe la UEFA.
Mwaka huo,
ilifanya maajabu kwa kuzifunga timu zenye majina Ulaya kama FC Lorient, Sparta
Prague na Olympique Lyonnais, kabla ya kufungwa katika Raundi ya Nne na FC
Porto ya Ureno, ambao walitwaa ubingwa wa michuano hiyo mwishowe.
Katika mchezo
wake wa kwanza wa kujipima nguvu, Yanga ilitoka 1-1 na DSC Arminia Bielefeld ya
Ujerumani, bao la timu hiyo ya Jangwani likifungwa na Tegete.
Kikosi cha
Yanga jana kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdu, Kabange Twite, Kevin Yondan,
Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Nurdin
Bakari, Jerry Tegete/Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi/Hamisi Kiiza na Simon Msuva.