Monday, January 21, 2013

KIIZA TAYARI KUREJEA UWANJANI

hamisi kiiza

Na Idrisa Bandali
KIPA wa tatu wa Yanga SC, Yussuf Abdul na mshambuliaji Mganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ waliokuwa wanasumbuliwa na Malaria, wamepona na leo wamefanya mazoezi na wenzao kwenye Uwanja wa Mabatini, Kijitonyama, Dar es Salaam.
Wawili hao walikosa mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Black Leopard ya Afrika Kusini juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambao timu yao ilishinda mabao 3-2.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizguto ameiambia SWIRARTY BLOG leo kwamba, timu imeendelea na mazoezi leo na wachezaji wote wameshiriki wakiwemo Abdul na Kiiza.
Alisema kwa sasa Yanga haina majeruhi hata mmoja na inaendelea vema na mazoezi yake kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu hya Vodacom Tanzania Bara unaoanza mwishoni mwa wiki.
Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, katika kujiandaa na mzunguko huo wa pili wa Ligi Kuu, waliweka kambi ya wiki mbili Jijini Antalya, Uturuki kuanzia Desemba 30 mwaka jana hadi Januari 12 mwaka huu.
Katika kambi hiyo, pamoja na kufanya mazoezi ya nguvu ya ufukweni, uwanjani na gym, Yanga ilipata mechi tatu za kujipima nguvu dhidi ya Ariminia Bielefed ya Daraja la Nne Ujerumani waliyotoka nayo sare ya 1-1, kabla ya kufungwa 2-1 na Denizlispor FC ya Daraja la Kwanza Uturuki na 2-0 na Emmen FC ya Daraja la Kwanza Uholanzi.
Yanga ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 29, baada ya kucheza mechi 13, ikifuatiwa na Azam iliyomaliza na pointi zake 24 na mabingwa watetezi, Simba SC waliomaliza na pointi 23.