|
azam fc na kombe lao la mapinduzi |
Na Idrisa bandali
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeipongeza uongozi wa
klabu ya Azam kwa timu yao kufanikiwa kutwaa Kombe la Mapinduzi mwaka huu.
Taarifa ya TFF, imesema kwamba Azam kufanikiwa kutetea
ubingwa huo inaonyesha jinsi klabu hiyo ilivyojipanga kabla ya kuingia katika
mashindano hayo ambapo ilicheza fainali dhidi ya Tusker FC ya Kenya.
“Pia ushindi huo utakuwa changamoto kwa timu nyingine za
Tanzania Bara zitakazopata fursa ya kushiriki michuano hiyo ya Kombe la
Mapinduzi mwakani. Michuano hiyo iko kwenye Kalenda ya Matukio ya TFF,”imesema
taarifa hiyo.
Azam FC Jumamosi usiku walitetea Kombe la Mapinduzi kwenye
Uwanja wa Amaan, Zanzibar baada ya kuifunga Tusker FC ya Kenya mabao 2-1.
Kwa ushindi huo, Azam walizawadiwa Sh. Milioni 10, wakati
washindi wa pili Tusker wamepata Sh. Milioni 5.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ramadhan Rajab Ibada
‘Kibo’ aliyesaidiwa na Mwanahija Makame Mfumo na Mgaza Kindundi, hadi mapumziko
hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao.
Azam ndio walioshambulia zaidi katika kipindi hicho, lakini
hawakuwa na bahati ya kufunga bao japo moja. Gaudence Mwaikimba alipewa pasi
nzuri na Brian Umony dakika ya 44, lakini shuti lake kali lilidakwa na kipa
Samuel Odhiambo.
Kipindi cha pili, Tusker walirudi na moto mkali na kuanza
kusukuma mashambulizi mfululizo langoni mwa Azam.
Hiyo iliwasaidia mabingwa hao wa Kenya kupata bao dakika ya
60, lililofungwa na Jesse Were aliyeunganisha kwa shuti kali la kimo cha mbuzi
pasi ya Robert Omunok.
Hata hivyo, bao hilo halikudumu sana, kwani Azam FC
walisawazisha dakika ya 72 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na beki Mkenya,
Joackins Atudo baada ya beki wa Tusker, Luke Ochieng kuunawa mpira kwenye eneo
la hatari.
Katika dakika mbili za nyongeza baada ya kutimu kwa dakika 90
za mchezo huo, alijitokeza binti mwenye umri kati ya 14 na 16 na kukatiza
uwanjani akitokea jukwaa la Urusi.
Refa refa Ramadhan Rajab Ibada ‘Kibo’ alijaribu kumsimamisha,
lakini aliendelea kukatiza Uwanja hadi nje ambako alipokewa na askari Polisi na
kutolewa nje kabisa ya Uwanja. Mtangazaji wa Uwanja wa Amaan, Farouk Karim
aliwatuliza mashabiki akisema binti huyo ametoroka hospitali ya vichaa, Kidongo
Chekundu na tayari Polisi wamemkamata na kumrejesha huko.
Hadi dakika 90 zinamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana
bao 1-1 na ndipo zikaongezwa dakika 30.
Gaudence Exavery Mwaikimba aliipatia Azam bao la ushindi
dakika ya pili tu tangu kuanza kwa muda wa nyongeza baada ya kuwazidi nguvu na
maarifa mabeki wa Tusker.
Aidha, Jesse Were mshambuliaji wa Tusker aliibuka mfungaji
bora kwa mabao yake matano na kuzawadiwa Sh. 300,000, akifuatiwa na Joackins
Atudo wa Azam aliyefunga mabao matatu sawa na Adeyum Saleh Ahmed wa Miembeni.