BINGWA wa 11
wa Kombe la Mapinduzi, anatarajiwa kupatikana leo kwenye Uwanja wa Amaan,
visiwani hapa wakati Tusker FC ya Kenya itakapomenyana na Azam FC ya Dar es
Salaam.
Azam FC ambao
ndio mabingwa watetezi wa michuano hii, waliingia fainali baada ya kuwatoa
Simba kwa penalti 5-4, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 120, wakati Tusker
dakika 90 ziliwatosha kuwang’oa Miembeni ya hapa kwa kuwachapa 2-0.
Mchezo huo
unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua kutokana na ubora wa soka wa timu zote
katika mashindano haya tangu yanaanza Januari 2, Tusker wakitokea A lililokuwa
na timu kali kama Simba na Jamhuri, Azam kundi B lililokuwa na timu kali pia za
Miembeni, Mtibwa Sugar na Coastal Union.
Nahodha wa
Tusker, Joseph Shikokoti amerudia kusema kwamba Azam hawatawazuia kutwaa Kombe
leo.
“Tutawafunga
Azam, hawawezi kutuzuia kutwaa hili Kombe, tumewaona wanavyocheza na tunakiri
ni timu nzuri, lakini tutawafunga tu,”alisema beki huyo wa zamani wa Yanga
alipozungumza na SWIRATY BLOG jana.
Kwa upande
wake, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Muingereza Kali Ongala amesema kwamba wana
matumaini ya kubeba Kombe la Mapinduzi leo, ingawa anakiri utakuwa mtihani
mzito kwa sababu wapinzani wao, Tusker FC ya Kenya ni timu nzuri.
Akizungumza
na SWIRATY BLOG jana, Kali alisema kwamba Wakenya wanawazidi Watanzania mambo
mengi sana kisoka, lakini kwa hali yoyote Azam itapambana kubakisha taji
nyumbani.
“Itakuwa
mechi ngumu, kama ulivyoiona Tusker ni timu nzuri kwa kweli, imekamilika kila
idara, lakini sisi pia tuna timu nzuri na tutapigana kufa na kupona,”alisema
mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga SC.
Pamoja na
hayo, Kali ameomba wapenzi wa soka Zanzibar kujitokeza kwa wingi leo uwanjani
kuishangilia Azam FC kwa sababu ni timu ya nyumbani, ili iweze kubakiza taji
hilo.
“Sisi ni
timu ya Tanzania, na Zanzibar ni sehemu ya Tanzania, hivyo tunaomba mashabiki
wajitokeze kwa wingi kutushangilia ili tuweze kubakiza taji hapa
nyumbani,”alisema.
Azam wanatumia
mfumo wa kushambulia moja kwa moja mipira mirefu na viungo wake karibu wote
wanakuwa na jukumu la kukaba zaidi ya viungo wa pembeni ambao hushambulia moja
kwa moja.
Tusker wao
wanapiga mipira mirefu na ni hatari sana kwa mipira ya kutokea pembezoni mwa Uwanja.
Timu zote
zina safu imara za ulinzi na kiungo na mabeki wake wana desturi ya kupanda
kusaidia mashambulizi wakati wa mipira ya kona kwenye lango la wapinzani.
Safu ya
ushambuliaji ya Azam leo itamtegemea Mganda Brian Umony kwani hakuna uhakika wa
Gaudence Mwaikimba kuanzishwa kutokana na kuonekana kupoteza nafasi nyingi za
kufunga katika mashindano haya, ambayo hadi sasa amefunga bao moja tu.
Tusker watakuwa
na kinara wa mabao wa mashindano haya, Jesse Were ambaye hadi sasa amefunga
mara nne.
Kwa ujumla,
kikosi cha Azam leo kinatarajiwa kuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Samir Hajji
Nuhu, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Uhuru Suleiman, Abdulhalim
Humud, Brian Umony, Humphrey Mieno na Uhuru Suleiman.
Tusker FC; Samuel
Odhiambo, Luke Ochieng, Bright Jeremiah, Mark Odhiambo, Joseph Shikokoti,
Frederick Onyango, Justine Monga, Khalid Aucho, Jesse Were, Ismail Dunga na
Robert Omonok.