Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akikata
utepe, kuzindua Mradi wa Kuinua Elimu ya Msingi ijulikanayo kama 'Tz 21
Century Basic Education Program, mradi uliofadhiliwa na Shirika la
Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID). Kulia ni Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi, Shukuru Kawambwa.Picha na Muhidin Sufiani-OMR
Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amezindua
Mradi wa Kuinua Ubora wa Elimu ya Msingi wa “TZ 21st Century Basic
Education Program”
Sherehe za uzinduzi wa
mradi huo ambao unalenga kuinua ubora ya elimu ya msingi kwa kutumia
teknolojia ya habari na mawasiliano umeanzishwa na Shirika la Kimataifa
la Maendeleo la Marekani (USAID) zimefanyika leo katika shule ya msingi
Kambarage mkoani Mtwara.
Akihutubia katika
uzinduzi huo Dk. Bilal aliwataka Watanzania kuendelea kujenga
imani na mfumo wa elimu uliopo nchini kwani ni mfumo bora ukilinganisha
na mifumo ya elimu iliyopo katika nchi nyingine za Kusini Mashariki mwa
Afrika.
Makamu wa Rais alisema kwa muda mrefu
sasa, imani imejengeka katika jamii kwamba elimu inayotolewa hapa nchini
ni duni na inahitaji kubadilishwa.
Aliwahakikishia
Watanzania kuwa elimu inayotolewa hapa nchini haijashuka kiasi hicho
kwani matokeo ya Utafiti wa Kufuatilia Ubora wa Elimu katika nchi za
Kusini Mashariki mwa Afrika (SACMEQ) ya mwaka 2000 na 2007 yanaonyesha
kuwa ukilinganisha na nchi nyingine, mfumo wa elimu hapa nchini ni bora.
“Kwa
mfano, kati ya nchi 15 zilizofanya utafiti huo, nchi yetu ilifanya
vizuri katika somo la Hisabati na Kusoma na kuwa kati ya nchi bora za
kwanza katika utafiti wa mwaka 2007,” alidokeza Dkt. Bilal.
Makamu
wa Rais pamoja na kukiri kwamba kuna watoto wachache
wanaomaliza darasa la saba bila ya kuwa na stadi za kusoma na kuandika
vizuri lakini alisema wapo wengi wanaomaliza na kufanya vizuri na
kuwasihi wananchi wasikatishwe tamaa na maoni ya watu mbalimbali kuhusu
kushuka kwa elimu nchini bali waongeze juhudi na kuwa na fikra chanya
katika kutoa elimu bora.
Dkt. Bilal alitumia
fursa hiyo pia kuwataka wadau wa elimu kulipa umuhimu wa pekee suala la
upimaji na utahini katika shule za msingi kwani mitihani bora bado ni
changamoto ambayo inahitaji kuangaliwa upya na wazazi na walimu kwa
upande wao wana jukumu la kuhakikisha watoto wanasoma maana elimu bora
ya msingi ndiyo itakayosaidia kuondokana na umaskini na kuwa na
maendeleo endelevu.
Akizungumza katika hafla
hiyo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa alisema
mradi huo utasaidia katika kufanikisha utekelezaji wa MMEM Awamu ya III
(2012-2016) hususan katika kuinua kiwango cha ubora wa
elimu ya msingi itolewayo nchini.
Naye Balozi
wa Marekani nchini Alfonso Lenhardt alielezea kufurahishwa kwake kwa
kuingizwa mradi huo katika utaratibu wa kutoa taarifa za elimu
(Education Management Information System) akiwa na matumaini kwamba
utasimamiwa na kuendelezwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.