Frank Lampard, Carles Puyol, David Villa na Ivica Olic ni Majina makubwa katika anga za Soka za Ulaya na Dunia nzima lakini wote hawa hawatakuwepo kwenye Vikosi vya Nchi zao zitakazocheza Fainali za EURO 2012 zinazoanza huko Poland na Ukraine Juni 8.
Wote hao ni majeruhi.
Olic ndie alieongezeka majuzi tu kwenye Listi ya Majeruhi ya Masupastaa na hivyo atakosa kuichezea Nchi yake Croatia.
Mabingwa wa Ulaya na Dunia, Spain, watawakosa Veterani wao Beki Carles Puyol na Straika hatari David Villa.
England wataikosa mihimili yao mikubwa
kwenye Kiungo baada ya Lampard na Gareth Barry wote kuumia huku Italy
itamkosa Straika Kijana Guiseppe Rossi.
Wenyeji Ukraine watamkosa Kipa Veterani
Oleksandr Shovkovsky wakati Russia itakuwa bila ya Mabeki Roman
Shishkin na Vasili Berezutski, na France itatinga EURO 2012 bila ya
Fowadi Remy Loic.
Italy bado wana wasiwasi na Beki Andrea
Barzagli ambae, ingawa bado yuko Kambini na Timu, lakini huenda
akazikosa Mechi zote za Makundi.
England nao bado wanae Wayne Rooney
licha ya kuzikosa Mechi mbili za mwanzo za Kundi lao dhidi ya Ufaransa
na Sweden kwa kuwa kifungoni na anaweza kucheza tu Mechi ya mwisho ya
Kundi dhidi ya Ukraine.
Mbali ya kuwakosa Lampard na Barry kwa
maumivu, juzi aliongezeka Sentahafu Gary Cahill ambae amevunjika Taya
na nafasi yake kuchukuliwa na Fulbeki Martin Kelly asie mzoefu na
kumwacha Sentahafu Veterani Rio Ferdinand na hilo kuzua mjadala mkubwa
huko England.
Akikiri pengo la Puyol na Villa, Kocha
wa Spain, Vicente del Bosque, amesema: “Hao wawili ni pengo kubwa kwetu
lakini tunao Wachezaji wazuri kwenye nafasi zao.”
Spain, ambao ndio Mabingwa Watetezi,
watacheza Mechi yao ya kwanza na Italia na mbali ya kupungukiwa
kutokana na majeruhi vile vile inabidi waipige kikumbo ile ‘laana” ya
Bingwa Mtetezi wa EURO kushindwa kutetea Taji lake tangu Mashindano
haya kuanzishwa Mwaka 1960.
Lakini nao wapinzani wao Italy, licha
ya pia kukumbwa na majeruhi, wanaingia kwenye Mechi hiyo huku wakiwa na
ukungu wa kashfa kubwa Kambini kwao baada ya Mchezaji wao mmoja
Domenico Criscito kudakwa na Polisi Kambini akihusishwa na tuhuma za
upangaji matokeo Mechi za Ligi huko Nchini Italia na kumfanya Criscito
aondolewe kwenye Kikosi.
Ingawa Timu zote 16 ambazo ziko Fainali
zimewasilisha Majina ya Vikosi vya Wachezaji wao 23 kwa UEFA hapo Mei
29, Siku ambayo ndio ilikuwa ya mwisho kufanya hivyo, Timu ambazo
zitapata majeruhi ziko huru kumbadili Mchezaji alieumia kabla ya
kucheza Mechi yao ya kwanza ikiwa tu kuumia huko kutathibitishwa na
Kamati ya Afya ya UEFA pamoja na Daktari wa Timu husika.