Sunday, June 3, 2012

UAMSHO ZANZIBAR WASALIM AMRI KWA POLISI

Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi Zanzibar
Wananchi wa Zanzibar wakiwemo wafuasi wa Kikundi cha Uamsho kilichotangaza kufanyika kwa mhadhara kwenye viwanja vya Lumumba mjini hapa, kimetii amri ya Jeshi la Polisi kwa kutoonekana kwa muumini ama viongozi wa kikundi hicho katika viwanja hivyo.
Afisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema leo kuwa, Jeshi la Polisi limeweza kudhibiti maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar na hivyo kutojitokeza tena kwa wafuasi wa kikundi hicho kama ilivyotangazwa awali.
Inspekta Mhina amesema Kikundi hicho cha Uamsho kupitia kwa Kiongozi wake Sheikhe Farid Hadi, juzi kilijigamba kufanya Mhadhara mkubwa leo arasili katika viwanja vya Lumumba mjini hapa hata baada ya Serikali kupiga marufuku mikusanyiko, kimeshindwa kufanya hivyo kufuatia agizo la Jeshi la Polisi lakuwataka wasitishe vinginevyo wangekabiliana na mkono wa dola.
Jana Kamishna wa Polisi Zanzibar CP. Mussa Ali Mussa, alitangaza kuupiga marufuko mhadhara huo na kuwataka wananchi na waumini kutohudhuria na kwa yeyote atakayekaidi agizo hilo angechukuliwa hatua kali.
Kufuatia agizo hilo, Polisi wa Operesheni maalum leo, walimwagwa katika viwanja vya Lumumba huku magari yenye askari wa kutuliza ghasia yakiranda kwa kila eneo kumkabili yeyote atakayekaidi na kufika kwenye viwanja hivyo kwa madhumuni ya kuhudhuria mhadhara huo.
Hatua hiyo ya Polisi imeweza kudhoofisha kabisa hali ya majigambo ya viongozi na wafuasi wa Kikundi hicho cha Uamsho waliotangaza kufanya mhadhara huo hata baada ya serikali kupiga marufuku.
Viongozi wa kikundi hicho ambao walionekana kugawanyika waliwajulisha baadhi ya wafuasi wao kuwa hali isingekuwa swari kwa upande wao kutokana na Jeshi la Polisi kusambaza makachero na askari wa kawaida katika maeneo mbalimbali ikiwemo Viwanja vya Lumumba palipopangwa kufanyika kwa mhadhara huo.
Ni wafuasi wachache tu walionekana kufika katika msikiti wa Mbuyuni kwa sala ya kawaida na pengine kupata taarifa za hatima ya mhadhara huo uliopigwa stop na Jeshi la Polisi.