Thursday, June 14, 2012

MBUNGE wa jimbo la Iramba magharibi (CCM) mkoani Singida, Mwigulu Nchemba, anakusudia kuwasilisha hoja binafsi katika  bunge la bajeti linaloendelea juu ya kuanzishwa kwa baraza maalum litakaloshughulikia makosa ya uhujumu uchumi na vitendo vya rushwa.
Amesema amefikia uamuzi huo ambao amedai utasadia kwa kiasi kikubwa wananchi kuendelea kuiamini serikali yao , baada ya kubaini kuwa kesi zinazohusu vitendo hivyo, huchukua muda mrefu, mno kumalizika na kitendo hicho,huchangia watuhumiwa wengi kuachiliwa huru.
Akifafanua zaidi, amedai kuwa kuchelewa kumalizika kwa kesi hizo, hutoa mwanya kwa watuhumiwa kutoa rushwa ili sheria iweze kupinduliwa kwa manufaa yao .
Mwigulu ambaye pia ni Katibu wa fedha na uchumi wa CCM taifa, amesema kuachiwa kwa watuhumiwa wa makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, kunachangia kuporomoka kwa maadili ya viongozi na wakati huo huo, wananchi kuichukia serikali yao.
Amesema mazingira ya usikilizaji wa kesi hizo yalivyo hivi sasa katika mahakama za kawaida, yanachangia kupunguza ufanisi wakati wa kuzishughulikia, kutokana na msongamano wa kesi katika mahakama hizo za kawaida.
Mwigulu amesema upo umuhimu mkubwa wa kuongeza adhabu ya makosa hayo ambayo itakuwa fundisho la kweli kwa wakosaji na kuwaogopa viongozi/wananchi wanaotarajia kutoa rushwa ua kuhujumu uchumi.